Arsenal wamzidi kete Man Utd, wapiga hatua kumnasa winga 'lulu' wa Leicester City
Arsenal kwa sasa ndiyo timu inayotazamwa na wengi kama moto wa kuotea mbali nchini Uingereza. Kitu cha kutisha zaidi kwa wapinzani wao ni kwamba mastaa wao wengi ndio kwanza wanaingia kwenye kipindi cha ubora wao wa juu zaidi kisoka.
Inaaminika kuwa kikosi hiki cha Mikel Arteta kikipewa nguvu kidogo tu, hasa kwenye safu ya ushambuliaji, kinaweza kutawala Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League) kwa miaka mingi ijayo ya muongo huu.
Hata hivyo, ili kuweka misingi ya utawala wa muda mrefu, Gunners hawatakiwi tu kuangalia mafanikio ya sasa, bali lazima waweke jicho lao moja kwenye siku zijazo. Hicho ndicho hasa wanachokifanya hivi sasa kwa kupambana kufa na kupona kumnasa winga chipukizi wa Leicester City, Jeremy Monga.
Kinda huyu mwenye umri wa miaka 16 anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji wenye vipaji vikubwa zaidi vya asili nchini Uingereza kwa sasa. Licha ya umri wake mdogo, tayari amecheza mechi 30 katika kikosi cha kwanza cha Leicester City msimu uliopita.
Bahati mbaya kwa Leicester, msimu wao ulimalizika kwa majonzi baada ya kushuka daraja hadi League One (Daraja la Kwanza). Kutokana na hali hiyo, ni wazi kuwa mchezaji mwenye kipaji kikubwa na uwezo kama wa Monga hawezi kubaki huko, na kuhama kwake ni jambo lisiliepukika.
Man Utd wanamtaka Monga, lakini Monga anaitaka Arsenal
Taarifa kutoka nchini Uingereza zilifichua kuwa Arsenal walikuwa kwenye vita kali na mahasimu wao wakubwa Manchester United katika mbio za kuwania saini ya Monga.
Mtaalamu wa masuala ya usajili, Graeme Bailey, alieleza kuwa maskauti wengi barani Ulaya tayari wanamchukulia Monga kama mmoja wa wachezaji bora zaidi wa kizazi hiki nchini Uingereza.
Wamiliki wapya wa Manchester United, kampuni ya INEOS, wamekuwa wakifanya jitihada kubwa za kusajili makinda wenye vipaji vya juu ili kujenga academy yao tangu walipochukua hatamu klabuni hapo. Hata hivyo, inaonekana Arsenal wamewapiku katika hili.
Mwandishi wa habari za michezo kutoka BBC, Sami Mokbel, alidokeza kuwa Monga mwenyewe yuko tayari kujiunga na Arsenal akivutiwa na mradi unaoendelea chini ya Arteta. Mokbel aliandika:
“Arsenal wamepiga hatua kwa ajili ya kumtaka mshambuliaji chipukizi wa Leicester, Jeremy Monga, 16, katika wiki za hivi karibuni. Monga anatajwa kama mmoja wa makinda bora zaidi katika soka la Uingereza na amekuwa akitolewa macho na klabu nyingi. Inaeleweka kuwa kinda huyo yuko tayari kujiunga na Arsenal, lakini kwa sasa haijulikani wazi kama kuondoka kwake Leicester kutahitaji uamuzi wa mahakama ya usuluhishi (tribunal).”
Arsenal waongeza kasi ya mazungumzo
Mwandishi wa habari za usajili anayeaminika, Ben Jacobs, amethibitisha kuwa Arsenal tayari wamefungua mazungumzo rasmi kwa ajili ya kukamilisha uhamisho huo. Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), Jacobs alifafanua:
“Arsenal wapo kwenye mazungumzo ya kumsajili Jeremy Monga. Klabu kadhaa kubwa zimeonyesha nia ya kumtaka winga huyo wa miaka 16 wa Leicester City. Vyanzo vinasema Leicester imepokea hadi ofa nane rasmi kutoka kwa klabu kubwa za Uingereza na barani Ulaya. Monga anaweza kugharimu zaidi ya pauni milioni 10. Kuna uwezekano uhamisho huu ukaamuliwa na kamati ya usuluhishi (tribunal) ili kupanga ada ya usajili.”
Katika taarifa mpya iliyotolewa Alhamisi mchana, Jacobs amethibitisha kuwa mazungumzo hayo sasa yamepiga hatua kubwa, huku Arsenal wakiongoza mbio hizo kwa kasi kubwa kuliko klabu nyingine zote.
Ripoti kutoka gazeti la The Sun zinasema kuwa uhamisho wa Monga utagharimu Arsenal kati ya pauni milioni 10 hadi pauni milioni 15, isipokuwa tu kama pande hizo mbili zimeshindwa kukubaliana na kesi hiyo kupelekwa kwenye kamati maalum ya usuluhishi wa ada za uhamisho kwa wachezaji chipukizi.