Sio Siri Tena! Arsenal 'Yatupa Karata' Yote kwa Morgan Rogers wa Aston Villa
Mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza, Arsenal, wameanza kufanya kweli sokoni baada ya ripoti kufichua kuwa wako kwenye hatua nzuri ya kumsajili kiungo mshambuliaji wa Aston Villa na timu ya taifa ya Uingereza, Morgan Rogers.
Chini ya kocha Mikel Arteta, Arsenal wametoka kwenye msimu wa mafanikio makubwa ambapo walitwaa taji la Premier League na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ili kuendeleza makali hayo, Mkurugenzi wa Michezo wa klabu hiyo, Andrea Berta, hana mpango wa kubweteka na anataka kuongeza nguvu mpya kikosini msimu huu.
Rogers Ndio Kipaumbele cha Kwanza cha Arteta
Mtaalamu wa masuala ya usajili wa wachezaji barani Ulaya, Fabrizio Romano, amefichua kuwa Arsenal wamedhamiria kwa dhati kumleta Rogers kwenye Uwanja wa Emirates na sasa mambo yanaenda kasi.
Kupitia chaneli yake ya YouTube, Romano ameeleza kuwa Rogers ndiye mchezaji anayesakwa kwa udi na uvumba na washika mitandao hao wa London.
“Nitaendelea kumtaja Morgan Rogers kama shabaha namba moja, mbili na tatu kwa Arsenal. Wanataka kumsajili kwa namna yoyote ile. Wamepiga hatua nzuri sana kwa upande wa mchezaji, hivyo Arsenal wanafanya kazi kubwa kufanikisha dili la kumsajili Morgan Rogers kutoka Aston Villa.”
Romano aliongeza kuwa mazungumzo yanaendelea vizuri na dili hilo liko hai kabisa kwa upande wa mchezaji, ambaye anavutiwa sana na mradi wa soka wa Arsenal baada ya mafanikio yao ya hivi karibuni.
Dau la Pauni Milioni 100 Mezani?
Hata hivyo, kibarua kigumu kinabaki kwa upande wa klabu na klabu. Aston Villa haitaki kumwachia kiungo huyo kirahisi, ambaye kwa sasa yuko na kikosi cha Uingereza kwenye michuano ya Kombe la Dunia.
Ripoti kutoka TEAMtalk zinasema Villa wanataka dau lisilopungua pauni milioni 100 ili kukubali kumuachia nyota huyo.
Mwandishi wa habari za usajili, Ben Jacobs, pia amethibitisha kuwa Arsenal wanatarajiwa kutuma ofa rasmi hivi karibuni baada ya kukubaliana na mchezaji huyo ambaye yuko tayari kutua Emirates.
“Morgan Rogers ndiye mchezaji anayeongoza kwenye orodha ya usajili ya Arsenal, na mchezaji mwenyewe ana shauku ya kuhamia hapo. Bando hakuna makubaliano rasmi na Aston Villa, lakini miamba hiyo ya London sasa inatarajiwa kutuma ofa yao hivi karibuni,” aliandika Jacobs kupitia mtandao wa X.
Vipi Kuhusu Bradley Barcola?
Arsenal pia wamekuwa wakihusishwa na winga wa Paris Saint-Germain, Bradley Barcola, ambaye pia ananyatiwa kwa karibu na mahasimu wao Liverpool.
Hata hivyo, Romano amesisitiza kuwa ingawa Barcola yumo kwenye rada za Arsenal, nguvu zao zote kwa sasa zimeelekezwa kwa Morgan Rogers, na dili la Barcola si la dharura kwa sasa.
Kazi kubwa sasa inabaki kwa Arsenal kukubaliana na Aston Villa kuhusu ada ya usajili ili kukamilisha usajili huo unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa klabu hiyo.