Chelsea yajipanga kunyakua saini ya Julian Alvarez, Arsenal nao hawajabaki nyuma
Vita mpya ya usajili jijini London
Klabu ya Chelsea imejiunga rasmi na mbio za kumsajili mshambuliaji matata wa Atletico Madrid, Julian Alvarez, katika kile kinachoonekana kuwa ni vita kubwa dhidi ya mahasimu wao wa London, Arsenal. Mshambuliaji huyu wa kimataifa wa Argentina kwa sasa anatafutwa na klabu nyingi kubwa barani Ulaya kufuatia hamu yake ya kutaka kuondoka nchini Uhispania.
Chelsea yatumia mwanya wa Nicolas Jackson
Taarifa kutoka kwa mwandishi wa habari za michezo, Nico Schira, zinaeleza kuwa Chelsea ilifanya mazungumzo na Atletico Madrid Alhamisi iliyopita jijini London. Inasemekana kuwa mazungumzo hayo hayakuhusu Alvarez pekee, bali pia hatima ya mshambuliaji wa Chelsea, Nicolas Jackson, ambaye yuko kwenye rada za klabu hiyo ya Uhispania.
Chelsea inaonekana kutaka kutumia fursa ya Atletico kumtaka Jackson ili kupunguza gharama za usajili wa Alvarez. Jackson kwa sasa amewekewa bei ya Pauni milioni 65 na Chelsea, jambo ambalo linaweza kuwa chachu ya kukamilisha dili hilo la kubadilishana wachezaji au kupunguza bei ya jumla ya mshambuliaji huyo wa Argentina.
Arsenal wapo tayari kuvunja benki
Licha ya Chelsea kuingia kwenye mchakato huo, Arsenal inaonekana kuwa na nia ya dhati kabisa. Ripoti zinaonyesha kuwa washika mitutu hao wa London wako tayari “kuvunja benki” ili kumsajili Alvarez. Mchambuzi wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, amethibitisha kuwa ndani ya Arsenal wanaamini wana uwezo wa kifedha wa kukamilisha dili hilo, hususan kama Gabriel Martinelli atakamilisha uhamisho wake kwenda Al-Hilal.
“Arsenal wanaamini ndani ya klabu kuwa wanaweza kumudu dili la Julian Alvarez. Hasa kama Gabriel Martinelli ataenda Al-Hilal, dili ambalo linaendelea kufanyiwa kazi,” alisema Romano.
Changamoto za kibiashara
Atletico Madrid inalindwa na mkataba wa Alvarez wenye kipengele cha kuvunja mkataba cha Euro milioni 500. Hata hivyo, klabu hiyo inatajwa kuhitaji kiasi cha Euro milioni 200 ili kumwachia staa huyo. Inasemekana pia kuwa Atletico ingependelea kumuuza mchezaji huyo nje ya La Liga.
Barcelona nao wanatajwa kuhusika kwenye sakata hili, hata hivyo, Alvarez ameshaweka wazi kuwa Barca ndiyo klabu yake ya ndoto, lakini matatizo ya kifedha ya Wakatalunya hao huenda yakawapa nafasi nzuri klabu za Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League) kuibuka washindi.
Kwa sasa, macho yote yako kwa Alvarez ambaye ameshaweka wazi nia yake ya kuondoka, huku Chelsea na Arsenal zikisubiri kuona nani atafanikiwa kushawishi dili hilo kabla ya dirisha la usajili kufungwa.