Skip to content

Federico Chiesa afunguka mustakabali wake Liverpool, ampa mchongo Curtis Jones kujiunga na Inter Milan

SokaNews
Updated: Published: Jumamosi, 6 Juni 2026 · 3 min read
liverpool federicochiesa curtisjones intermilan epl tetesizausajili
Federico Chiesa afunguka mustakabali wake Liverpool, ampa mchongo Curtis Jones kujiunga na Inter Milan

Mshambuliaji wa pembeni wa klabu ya Liverpool, Federico Chiesa, amefunguka kuhusu mustakabali wake ndani ya klabu hiyo na kuweka wazi sharti ambalo linaweza kumlazimu kufungasha virago vyake. Wakati huohuo, nyota huyo wa kimataifa wa Italia ametoa ushauri kwa kiungo mwenzake wa Liverpool, Curtis Jones, anayehusishwa na mipango ya kujiunga na miamba ya soka ya Italia, Inter Milan.

Chiesa alijiunga na Liverpool akitokea Juventus kwa ada ya takriban pauni milioni 12.5 wakati wa dirisha la usajili la majira ya joto mwaka 2024. Licha ya matumaini makubwa yaliyokuwepo wakati akitua Anfield, mambo hayajawa mazuri kwa mchezaji huyo wala kwa klabu, huku akishindwa kupata nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza katika misimu miwili iliyopita.

Kutokana na hali hiyo, Chiesa sasa anakiri kuwa atalazimika “kutazama kwingine” iwapo hatapata uhakika wa kucheza kutoka kwa kocha mpya wa Liverpool, Andoni Iraola.

Sharti la Chiesa Kubaki Liverpool

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 ameeza wazi kuwa lengo lake kubwa ni kucheza soka la ushindani kila wiki, jambo ambalo amelikosa tangu atue nchini Uingereza.

“Nataka kucheza mara kwa mara. Kama sitapata nafasi ya kucheza mfululizo kwenye Ligi Kuu ya Uingereza, itabidi nitafute timu nyingine,” alisema Chiesa.

“Katika mwaka wangu wa kwanza Liverpool, kiuhalisia sikucheza kabisa… Nitakwenda kwenye ziara ya maandalizi ya msimu mpya nchini Marekani, kisha nitazungumza na klabu pamoja na kocha mpya Iraola, na baada ya hapo tutaona nini kitatokea.”

Akizungumzia kuhusu maisha yake ya zamani ndani ya klabu ya Juventus, Chiesa alionyesha bado ana mapenzi makubwa na klabu hiyo ya Turin na kueleza kuwa hakuondoka kwa kupenda.

“Juventus itakuwa moyoni mwangu daima, na ningependa kurejea huko siku moja. Sikuwahi kujadili masuala ya fedha na Juventus, na sitawahi kufanya hivyo—nisingewahi kuondoka klabuni hapo.”

“Sikuwahi kupewa ofa ya mkataba mpya. Thiago Motta na Giuntoli waliniambia wazi kuwa nitafute klabu nyingine ya kwenda.”

Ushauri kwa Curtis Jones Kuhusu Inter Milan

Mbali na mustakabali wake, Chiesa pia amefichua mazungumzo yake na kiungo wa Liverpool, Curtis Jones, ambaye naye anatajwa kuwa kwenye rada za mabingwa wa Italia, Inter Milan.

Chiesa amebainisha kuwa alimpa Jones picha halisi ya maisha ya soka nchini Italia na kumhimiza kuchangamkia fursa hiyo ikiwa itatokea.

“Jones aliniuliza jinsi maisha ya Italia yalivyo,” alifichua Chiesa.

“Nilimwambia kuwa maisha ya kule ni mazuri mno na hali ya hewa ni nzuri sana kuliko ya Liverpool. Curtis ana uwezo mkubwa sana wa kiufundi, na Inter Milan wapo sahihi kabisa kufikiria kumsajili.”

Rossi Amtabiria Makubwa Chiesa Newcastle United

Wakati Chiesa akihusishwa na uwezekano mkubwa wa kurejea nyumbani Italia msimu huu, aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Giuseppe Rossi, anaamini kuwa winga huyo anaweza kung’ara zaidi akijiunga na timu ya Newcastle United.

Akizungumza na mtandao wa Ozoon, Rossi alisema:

“Namwona Chiesa akifanikiwa sana kwenye timu kama Newcastle. Federico anahitaji kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara na mazingira sahihi ili kuonyesha kile anachoweza kufanya.”

“Ana mengi ya kuthibitisha na bado ana uwezo mkubwa wa kutoa mchango uwanjani, lakini kila kitu kinategemea yeye mwenyewe. Tunatumai anaweza kurejesha makali yake yaliyotufanya tushinde Euro mwaka 2020; alikuwa nguzo muhimu sana kwetu.”

Rossi aliongeza kuwa bado anamchukulia Chiesa kama mmoja wa mawinga bora duniani, licha ya kupitia kipindi kigumu hivi karibuni, na ana imani kubwa kuwa atarejea kwenye kiwango chake bora iwapo atapata mazingira sahihi ya kurejesha ari yake ya ushindani.