Skip to content

UCHAGUZI REAL MADRID: Riquelme Anyanyua Jezi ya Haaland, Aahidi Kumleta na Rodri Huku Perez Akimrudisha Mourinho

SokaNews
Updated: Published: Alhamisi, 4 Juni 2026 · 4 min read
realmadrid erlinghaaland rodri josemourinho florentinoperez laliga
UCHAGUZI REAL MADRID: Riquelme Anyanyua Jezi ya Haaland, Aahidi Kumleta na Rodri Huku Perez Akimrudisha Mourinho

Kuelekea uchaguzi mkuu wa Real Madrid unaotarajiwa kufanyika Jumapili hii, kampeni zimepamba moto huku wagombea wakishindana kutoa ahadi nzito ili kuwashawishi wanachama wapiga kura. Mgombea urais, Enrique Riquelme, amefanya kufuru baada ya kunyanyua jezi ya miamba hiyo ya Hispania ikiwa imeandikwa jina la mshambuliaji wa Manchester City, Erling Haaland, akiahidi kumshusha mchezaji huyo pamoja na kiungo Rodri iwapo atafanikiwa kushinda kiti hicho.

Riquelme anachuana vikali na rais wa sasa, Florentino Perez, katika uchaguzi huo ambao utawashirikisha takribani wanachama 95,000 waliojisajili (socios) kupiga kura kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006. Riquelme alionekana kwenye kipindi maarufu cha televisheni cha ‘El Hormiguero’ siku ya Jumatano kujaribu kujizolea umaarufu kwa wapiga kura hao.

Perez Amrudisha Jose Mourinho Kujibu Mapigo

Kwa upande wake, Florentino Perez hajaacha mambo yaende hivi hivi. Timu ya kampeni ya Perez imethibitisha kuwa kocha wa zamani wa timu hiyo, Jose Mourinho, aliyewahi kuinoa Madrid kati ya mwaka 2010 na 2013, atarejea kikosini kama kocha mkuu iwapo Perez atashinda kura za Jumapili. Video fupi ikimwonyesha Mourinho akitabasamu akiwa na jezi ya Real Madrid na kusema “ndiyo” ilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Perez aliliambia gazeti la AS:

“Mashabiki wa Real Madrid wanapaswa niamini. Nawaahidi kuwa tutakuwa na timu imara sana. Sitasita kusajili wachezaji na kuimarisha kila nafasi.”

Tayari Real Madrid imeshathibitisha kumsajili beki Ibrahima Konate kama mchezaji huru baada ya mkataba wake na Liverpool kumalizika, huku wakiactivate kipengele cha usajili cha Euro milioni 20 cha beki Denzel Dumfries kutoka Inter Milan. Perez pia amesisitiza kuwa nyota watatu; Kylian Mbappe, Jude Bellingham, na Vinicius Junior watabaki Bernabeu licha ya tetesi kuwa mmoja wao angeondoka msimu huu.

Mipango ya Riquelme na Kukataliwa kwa Mourinho

Hata hivyo, Riquelme ameweka wazi kuwa Jose Mourinho hatakuwa sehemu ya mradi wake iwapo atachaguliwa kuwa rais mpya wa klabu hiyo.

“Ni kocha mzuri, lakini mtindo wake wa ufundishaji ni tofauti kabisa na kile tunachokitafuta kwenye mradi wetu. Hatumtaki kwenye mradi wetu. Nina kocha mwingine kichwani.”

Badala yake, Riquelme amepanga kuwaleta magwiji wa zamani wa klabu hiyo, Raul Gonzalez kama Mkurugenzi wa Michezo na Fernando Hierro kama mkuu wa akademi ya vijana, akidai kuwa uwepo wao utalinda heshima na masilahi ya klabu.

Ahadi ya Haaland na Rodri, na Ahadi ya Kulipa Ada za Wanachama

Wiki iliyopita, Riquelme aliiambia ESPN kuwa kiungo wa Man City na mshindi wa Ballon d’Or, Rodri, ambaye amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake, ni aina ya mchezaji anayepaswa kucheza Real Madrid. Siku ya Jumatano alisisitiza zaidi kuhusu mpango huo:

“Ni mchezaji mkubwa, anayecheza nafasi ambayo Madrid inahitaji kuimarishwa. Tumeshaongea na wakala wake. Tunapaswa kuiheshimu klabu yake, lakini nikiwa rais atachezea Madrid. Nitafanya kila liwezekanalo.”

Riquelme alikwenda mbali zaidi na kutoa ahadi ambayo itamgharimu mfuko wake iwapo atashindwa kuitimiza:

“Erling Haaland na Rodri watakuwa sajili zangu za kipekee nikichaguliwa kuwa rais. Nisipotimiza ahadi yangu kwa yeyote kati ya wachezaji hawa, nimesaini makubaliano ya kisheria ambapo nitalipa asilimia 100 ya ada za uanachama wa klabu kwa msimu ujao. Haaland ana kipengele cha kuvunja mkataba, na anataka kuja Madrid.”

Kambi ya Haaland Yakanusha Vikali

Licha ya mbwembwe hizo za Riquelme, ukweli wa mambo unaonekana kuwa tofauti. Haaland alisaini mkataba mrefu na mnono na Manchester City mnamo Januari 2025 unaomfunga klabuni hapo hadi mwaka 2034. Inaripotiwa kuwa mkataba huo mpya uliondoa kipengele chochote cha ununuzi (buyout clause) kilichokuwepo awali.

Kufuatia kauli hizo za Riquelme, baba mzazi wa Haaland, Alfie Haaland, pamoja na wakala wa mchezaji huyo, Rafaela Pimenta, walitoa taarifa ya pamoja kukanusha madai hayo:

“Yote haya yanafurahisha sana lakini si kweli. Tunawatakia kila la heri wagombea wote wawili kwenye uchaguzi wa Real Madrid.”

Mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, pia ameeleza kuwa Manchester City haina wasiwasi wowote kuhusu mustakabali wa Haaland na haitegemei kuondoka kwake msimu huu, kwani mshambuliaji huyo ni nguzo muhimu katika mradi wa sasa chini ya kocha Enzo Maresca.